JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Tunamuomba Allah Atubariki sote na Atupe hima katika Dini Yake. Wasiwasi mara nyingi unatokana na shetani aliyelaaniwa, kwani Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: “Na shari ya wasiwasi wa Shetani, Khannaas. Anaye tia wasiwasi katika vifua vya watu, Kutokana na majini na wanadamu” (114: 4 – 6). Hivyo unapopata pepesi za shetani au wasiwasi kama huo unatakiwa useme Audhu Billaahi minash Shaytwaanir Rajiym (Najilinda kwa Allah kutokana na shetani aliye laaniwa). Bila ya shaka wasiwasi huo utaondoka. Usimpe shetani nafasi ya kukuchezea. Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: “Na uchochezi wa Shetani ukikuchochea basi omba ulinzi wa Allah. Hakika Yeye ni Msikizi, Mjuzi. Hakika wale wamchao Mungu, zinapowagusa pepesi za Shetani, mara huzindukana na hapo huwa wenye kuiona haki” (7: 200 – 201). Kwa kawaida shetani anataka kukushughulisha kwa mambo ambayo si ya msingi ili kukupotezea wakati wako ambao ni muhimu au ufanye jambo ambalo si muhimu. Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kinachoweza nafsi hiyo. Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Hakuweka uzito wowote katika Dini (22: 78). Unachotakiwa kuondoa katika najisi ni ile unayoiona, ile ambayo hujaiona au kuisikia harufu basi si juu yako kujitia wasiwasi. Toa wasiwasi wote juu ya najisi kama hizo mpaka ujue uhakika wake. Wakati mmoja ‘Umar ibn al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa anapita na mwenzake mara yakamwagwa maji kutoka juu ya nyumba. Yule bwana akaanza kuuliza kama yale maji ni ya najisi, ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alimkemea kuhusu hilo na akamkanya kuuliza, kwani kufanya hivyo ni kujitia katika mashaka.