Wakati Wa Swalah Ya Tahajjud Na Vipi Kuswali


972

SWALI: Swala ya Tahajjud inaswaliwa vipi? Na wakati gani? Je unaweza kutumia saa yake ikuamshe ili upate kuswali au mpaka uamke mwenyewe?

JIBU: AlhamduliLLaah - Sifa njema zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. Swalaah ya Tahajjud ni Swalaah inayoswaliwa usiku ambayo pia kwa jina lengine ni Qiyaamul-Layl (kusimama kuswali usiku). Nayo huswaliwa wakati wowote baada ya Swalah ya 'Ishaa mpaka karibu na Alfajiri. Ama ikiwa mtu anataka kupata fadhila zilizotajwa kuswali katika thuluthi ya usiku kama ilivyo katika Hadiythi ifuatayo: عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim] basi wakati huu wa Thuluthi ya mwisho ni kugawa sehemu tatu kuanzia Swalaah ya Magharibi mpaka Swalaah ya Alfajiri. Sehemu ya tatu ndio Thuluthiy-Llayl (thuluthi ya usiku) ya mwisho Na huswaliwa ifuatavyo: 1-Idadi ya Swalaah za Sunnah za usiku: Jumla ya Swalaah za usiku za Sunnah ni Raka'ah kumi na moja kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali usiku Raka'ah kumi na akitoa salaam baada ya kila Raka'ah mbili kisha akiswali Witr Raka'ah moja.” [Muslim] Na akasema vile vile: ”Hajapata Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuzidisha katika Ramadhwaan wala miezi mingine zaidi ya Raka'ah kumi na moja, akiswali nne, wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali nne wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali tatu.” [Al-Bukhaariy na Muslim] b-Namna zinavyoswaliwa Swalaah za usiku: Unatoa salaam kila baada ya Raka'ah mbili kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo: ((Swalaah ya usiku ni (raka’ah) mbili mbili na ukiogopa kukukuta asubuhi basi Swali Witr [Raka'ah] moja)) [Al-Bukhaariy] c-Suwrah za kusoma katika Swalash ya usiku: Hakuna Suwrah maaluum ya kusomwa katika Swalaah za usiku, bali ni vizuri sana kusoma Suwra ndefu kwa dalili ya Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) iliyotangulia juu kwamba: “Wala usiniulize uzuri wake.” akikusudia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Swalaah kwa utulivu kabisa kwa kusoma mara nyingine Suwrah ndefu, Rukuu ndefu, sujuwd ndefu na kadhalika. Pia kutokana na Hadiyth inayojata fadhila za kusoma Aayah nyingi katika Swalaah za usiku: ((Atakayesimama (usiku) na Aayah kumi hatoandikiwa katika miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kwa Aayah mia ataandikiwa ni miongoni mwa watiifu, na atakayesimama kwa Aayah elfu ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi)) [Abuu Daawuwd na amesahihisha Al-Albaaniy] Maana ya mirundi ni: Mirundi ya thawabu. Ama katika Raka'ah tatu za mwisho imethibitika kuwa alikuwa akisoma Suwrah zifuatazo: Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika Raka'ah ya mwanzo ya (Swalaah) Witr “Sabbihisma Rabikal-A'alaa” na Raka'ah ya pili “Qul-Yaa-Ayyuhal-Kaafiruwn” na Raka'ah ya tatu “Qul- Huwa-Allaahu Ahad pamoja na Qul-A'uwdhu mbili (Al Falaq na An Naas)” [At Tirmidhiy] Raka'ah hizi tatu za mwisho vile vile ziswaliwe mbili kwanza kisha umalizie na moja pekee, na katika hiyo raka’ah ya mwisho bada ya kuinuka katika ruku'u usome du'aa ya Qunuwt. Au pia unaweza kuziswali zote tatu kwa Tashahhud moja ya mwisho na kisha kutoa salaam, yaani bila kusoma At-Tahiyaat kwenye raka’a ya pili, na ‘Ulamaa wamesema kusema kuunga raka’ah tatu kwa pamoja ni kuitofautisha na Swalash ya Maghrib ambayo unakaa At-Tahiyaat kwenye raka’ah ya pili. Swali kuhusu kuweka saa au kuamka mwenyewe, jibu ni kwamba hakuna shuruti ya kuweka saa, vyovyote utakavyoamka kuswali ni sawa fadhila zake ni zile zile. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Tabia za Utume.