Zakaah Inafaa Kutolewa Ikiwa Mtu Ana Madeni?


314

SWALI: Swali langu ikiwa una madeni yafaa utowe zakaah ya mali shukran nasubiri majibu ndugu zangu Inshaallah. Allaah Barik

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali hili muhimu. Zakaah ni amana na haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) aliyopatiwa mja. Hivyo ni vyema uwe ni mwenye kuitoa katika maisha ya hapa duniani. Hakika swali lenyewe lina pande kadhaa na hivyo itakuwa vyema tuzitazame sehemu zote hizo ili tupate muongozo muafaka. Swali hili limeeleweka kwa pande mbili kila moja lina muongozo wake. Ikiwa wewe ndio unadaiwa na watu au mtu huna Zakaah unazotakiwa kutoa ila tu utakapokuwa na pesa nyingine zinazofika Niswaab. Kwa mfano, ikiwa una shilingi milioni moja ya Tanzania nawe wadaiwa shilingi laki tano. Baki uliyonayo ambayo ni laki tano ikiwa inafika Niswaab na ikapitiwa na mwaka mzima wa Kiislamu utafaa uilipie hiyo pesa Zakaah. Lakini kwa kawaida wenye madeni huwa si wenye uwezo wa kuwa na pesa hiyo. Hivyo, kanuni iliyowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) ni kuwa wenye madeni wapewe Zakaah ili watoke katika madeni hayo. Anasema Aliyetukuka: “Wa kupewa sadaka (Zakaah) ni mafakiri, masikini, wanaozitumikia, wa kutiwa nguvu nyoyo zao, katika kukomboa watumwa, wenye madeni, katika Njia ya Allaah na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaridhiwa na Allaah. Na Allaah ni Mwenye kujua, Mwenye hikima” (9: 60). Ikiwa wewe ndiye mwenye kudai watu wengine na hayo madeni yanafika Niswaab na kupitiwa na mwaka mzima kutakuwa na hali mbili. Hali ya kwanza ikiwa hizo pesa utazipata unapozihitajia basi utazilipia Zakaah lakini ikiwa ni madeni ambayo huwezi kuyapata kwa unaowadai basi hakutakuwa na Zakaah juu yako. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Ibrahim al-Dosari