Zakaah Kwa Vitu Vya Matumizi Kama TV, Komputa n.k


279

SWALI: Assalamu alakykum; Natanguliza Shukrani kwa Allaah (Subhanahu wataala) kutupa neema ya uhai na kuwawezesha ndugu zetu kubuni na kuendeleza mtandao wenye manfaa kede kede. Allaah (Subhanahu wataala) ndiye mlipaji. Nimejaribu kutafuta masuala kuhusu Zakaah humu ndani ya mtandao sikufanikiwa hata kwenye viungo mlivyoweka sijafanikiwa pia. Naomba mtuwekee darsa hii muhimu. Na kama ipo naomba nielekezwe. Suala langu ni kuwa hizi mali tunazonunua na kukaa nazo kama TV, computer n.k Jee zinatolewa Zakaa na kwa kiwango gani? JazaaKaAllaah

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani kwako ndugu yetu mpenzi kwa swali lako hili kuhusu mas-ala ya Zakaah. Ni maarufu kuwa Zakaah ni nguzo ya tatu ya Uislamu. kwa umuhimu mkubwa uliokuwa nao nguzo hii imefungamanishwa na nguzo ya pili, Swalah. Mfano ni, “Ambao huamini ghaibu na husimamisha Swalah na hutoa katika yale Tuliyowapa” (2: 3). Zakaah inamtakasa mwenye kutoa mwanamme au mwanamke, kwani Allaah Aliyetukuka Anasema: “Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo sadaka” (9: 103). Kuzuia kutoa Zakaah ni madhambi makubwa. Zakaah kama nguzo au Ibaadah nyengine yoyote katika Uislamu ina muongozo wake na masharti yake. Miongoni mwa hayo masharti ni: 1- Kupita hawl, yaani mwaka mmoja katika kalenda ya Kiislamu. 2- Kufika nisaab, yaani kiwango cha mali kinachomuwezesha mtu kutoa Zakaah. Miongoni mwa vitu ambavyo vinatolewa Zakaah ni: 1- Dhahabu na fedha: Mbali na hivyo ni vitu vyengine vinavyo tathminiwa kwavyo miongoni mwa bidhaa za biashara katika hukumu ya hizo, miongoni mwa madini na mali. Kwa sasa pia nyaraka zinaingia kwazo. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na wale ambao wanalimbikiza dhahabu na fedha wala hawazitolei Zakaah katika njia ya Allaah, basi wape habari ya adhabu iumizayo” (9: 34) 2- Wanyama: Hao ni ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka: “Enyi mlioamini! Toeni katika vile vizuri mlivyovichuma na katika vile Tulivyokutoleeni katika ardhi” (2: 267). 3- Matunda na nafaka: Nafaka ni kila chenye kuwekwa akiba chenye kuliwa kama vile ngano, shairi, fiwi, kunde, maharage, mtama, mahindi, mpunga na kadhalika. Ama matunda ni kama vile tende, zaituni na zabibu na kadhalika. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake” (6: 141). Ama kuhusu mali zisizopaswa kutolewa Zakaah ni: 1- Watumwa, farasi, nyumbu, punda kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Haipasi sadaka kwa mja mtumwa, farasi wake na kijana wake…” (Ahmad). 2- Mali ambayo haikufikia kiwango, isipokuwa mtu akipenda kujitolea. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Haipasi Zakaah kwa ngamia walio chini ya watano” (al-Bukhaariy na Muslim). 3- Vifaa ambavyo vipo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ambavyo si kwa ajili ya biashara. Mfano wa vifaa hivyo ni kama godoro, televisheni, kompyuta, gari, vyombo vya nyumbani na kadhalika. Hivyo havikutajwa katika sharia hivyo havimo katika vile vitu vinavyofaa kutolewa Zakah. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho: